Mkutano Mkuu wa 37 wa AU wamalizika kwa kuainisha vipaumbele vya Afrika vya mwaka 2024 na kuendelea
2024-02-20 09:11:44| CRI

Mkutano wa Baraza Tendaji la 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) ulimalizika Jumapili kwa kuainisha vipaumbele vya Afrika vya mwaka 2024 na kuendelea.

Mkutano huo ulifanyika chini ya kaulimbiu ya "Mwelimishe Mwafrika afae katika Karne ya 21: Kujenga mifumo thabiti ya elimu kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa elimu jumuishi, ya maisha yote, yenye ubora na inayofaa barani Afrika."

Wakati Afrika ikiangazia elimu katika mwaka 2024, mkutano huo ulijadili namna ya kuimarisha elimu na ujuzi ili kukidhi dira ya bara hilo na mahitaji ya soko. Baraza hilo, ambalo ni chombo cha juu zaidi cha kufanya maamuzi cha AU, liliangazia mafanikio na mapungufu yaliyobainishwa katika muongo wa kwanza wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa bara la Afrika wa miaka 50, Ajenda ya 2063.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat aliangazia baadhi ya maswala muhimu yanayolikabili bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kitaasisi, hatari za amani na usalama, athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, ukosefu wa usimamizi wa kiuchumi, changamoto za ushirikiano wa bara, na umaskini, miongoni mwa mambo mengine.