BoT yasema mtazamo wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2024 bado ni thabiti
2024-02-20 09:10:19| CRI

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa mtazamo wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2024 unatarajiwa kuendelea kuwa imara.

Katika Taarifa yake ya Sera ya Fedha ya Mapitio ya Katikati ya Mwaka 2023/2024, BoT ilisema ukuaji wa mapato katika Tanzania Bara unatarajiwa kufikia takribani asilimia 5.5 mwaka 2024, huku uchumi wa Zanzibar ukitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 7.4.

Taarifa hiyo ilisema uwekezaji wa umma na wa kibinafsi, mageuzi ya kuboresha mazingira ya biashara, na kurejea tena kwa shughuli za utalii zinatarajiwa kuchangia pakubwa katika makadirio ya ukuaji.

Aidha, taarifa hiyo pia imesema mvua zinazoendelea kunyesha kwa uwiano, zitachangia vizuri katika ukuaji wa mapato. Hata hivyo, ilisema hatari kuu kwa mtazamo wa ukuaji ni mivutano ya kijiografia na sera ya fedha inayoimarishwa katika nchi zenye uchumi wa juu.