Serikali ya Tanzania kuendeleza umeme wa jotoardhi
2024-02-21 23:11:23| cri

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Doto Biteko amesema Serikali ya Tanzania imeamua kwa dhati kuendeleza vyanzo vya umeme wa Jotoardhi ili kuhakikisha Tanzania inazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Dk. Biteko amesema hayo mara baada ya kukagua vyanzo vya jotoardhi vya Kiejo-Mbaka (60MW) na Ngozi (MW 70) mkoani Mbeya, na kusema vyanzo hivyo vya umeme vitaongeza nguvu katika vyanzo vilivyopo vya maji na gesi asilia.

Amesema ni lazima miradi ya Jotoardhi ianze, na wataanza na megawati 10 katika eneo la Kiejo-Mbaka na Ngozi huku nyingine zikifuata, na hii inajumuisha miradi mingine kama wa umeme wa jua wa eneo la Kishapu (150 MW) ambao umeanza kutekelezwa, miradi ya umeme wa upepo wa  Makambako na mradi wa Malagarasi ambao mkandarasi ameshasaini mkataba tayari kwa kuanza kazi.