Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye UM asema pingamizi ya kusitisha mapigano Gaza ni sawa na leseni ya kuua
2024-02-21 09:09:02| CRI

Kufuatia kura ya turufu ya Marekani juu  ya rasimu ya azimio la Baraza la Usalama ambayo inataka kusitishwa mapigano huko Gaza mara moja, mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Zhang Jun amesema pingamizi ya kusitisha mapigano huko Gaza haina tofauti na kuruhusu kuendelea kwa mauaji.

Akitoa ufafanuzi baada ya rasimu ya azimio hilo kupigiwa kura 13 za ndio kati ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama, ambapo Uingereza ilijizuia, Balozi Zhang, amesema China inaeleza kusikitishwa kwake na kutoridhika na kura ya turufu ya Marekani.

Ameongeza kuwa Algeria, kwa niaba ya mataifa ya Kiarabu, iliwasilisha rasimu ya azimio hilo na kwa kuzingatia mahitaji ya chini ya binadamu, linahitajika haraka kutokana na hali iliyopo na linastahili kuungwa mkono na wanachama wote wa Baraza la Usalama.

Hivyo amesema China inaitaka Israel kutii wito wa jumuiya ya kimataifa, kuachana na mipango yake ya kuishambulia Rafah, na kukomesha kuwaadhibu watu wa Palestina. China pia inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunganisha juhudi zote za kidiplomasia ili kuwapa watu wa Gaza nafasi ya kuishi, kuwapa watu wa eneo zima la Mashariki ya Kati nafasi ya kuwa na amani, na kutoa fursa ya haki kutendeka.