Benki ya Dunia yaipatia Zambia na Tanzania dola milioni 270 ili kuboresha uchukuzi na muunganisho wa biashara
2024-02-22 09:15:06| CRI

Benki ya Dunia imezipa Zambia na Tanzania ruzuku ya dola za Kimarekani milioni 270 kusaidia kuboresha uchukuzi na biashara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatano, fedha hizo zinakusudiwa kuboresha usafirishaji na mawasiliano ya biashara kwenye ukanda wa Dar es Salaam kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni sehemu ya mradi wa miaka sita wa Ukanda wa Usafiri wa Kuhimili Uchumi, unaolenga kuongeza ufanisi, uunganishaji na ustahimilivu wa hali ya hewa katika usafirishaji muhimu wa kikanda na njia za biashara za mashariki na kusini mwa Afrika.

Meneja wa Benki ya Dunia nchini Zambia, Achim Fock, alisema katika taarifa kwamba mradi huo ni dhamira kubwa ya biashara na usafirishaji wa kikanda, na kuongeza kuwa sekta za usafirishaji na ugavi zinatarajiwa kupata msukumo kutokana na shughuli husika zinazolenga kujenga uwezo wa kitaasisi na kisekta.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi huo utawanufaisha watu 2,500,000 nchini Zambia.