Takriban Wapalestina 17 wameuawa na wengine zaidi ya 34 kujeruhiwa katika shambulio la anga la Israel kwenye nyumba iliyopo katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Vyanzo vya matibabu vya huko pia vimeliambia Shirika la Habari la China Xinhua kwamba juhudi za uokoaji bado zinaendelea, na waliojeruhiwa ni pamoja na wanawake na watoto. Wahanga wote waliopatikana wamehamishiwa katika Hospitali ya Al-Aqsa.
Mashuhuda waliiambia Xinhua kwamba ndege ya kivita ya Israel ilirusha makombora kadhaa kwenye nyumba hiyo iliyokuwa ikihifadhi familia kadhaa zilizopoteza makazi.
Mlipuko huo mkubwa uliangusha jengo hilo na kusababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba za jirani katika eneo la magharibi mwa kambi hiyo.
Wakati huo huo, kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas, hadi kufikia siku ya Jumatano, idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza ilikuwa imefikia 29,313, huku wengine 69,333 wakijeruhiwa.