Zanzibar yapiga hatua katika kukuza utalii
2024-02-22 09:16:06| CRI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Hussein Ali Mwinyi alisema Jumatano kwamba serikali yake inachukua hatua za kuimarisha utalii visiwani humo.

Akihutubia katika ufunguzi wa Mkutano wa pili wa Kimataifa wa sekta ya utalii na maonesho (The Z-Summit, 2024), Mwinyi alisema hili ni tukio muhimu sana ambapo viongozi wa sekta ya utalii wanaungana na washawishi na wajasiriamali wa utalii wa ndani, Afrika Mashariki na kimataifa. Alibainisha kuwa serikali ya Zanzibar imeendelea kuwa imara katika dhamira yake ya kuendeleza miundombinu na mifumo ya usimamizi ambayo ndiyo msingi wa sekta ya utalii.

Aidha amesema serikali inawekeza zaidi katika kujenga barabara mpya, kuboresha usambazaji wa umeme, kuendeleza mipango ya udhibiti taka, na kufanya mradi kabambe wa ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Pemba.

Mwinyi alisema juhudi hizo zinalenga kuboresha ufikiaji, muunganisho, na uzoefu katika Zanzibar nzima, akiongeza kuwa juhudi za kulinda maeneo ya urithi zinaendelea.