UNESCO yapongeza uamuzi wa AU wa kuhimiza elimu mwaka 2024
2024-02-22 09:22:58| CRI

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) Jumatano lilipongeza uamuzi wa Umoja wa Afrika (AU) wa kuhimiza elimu mwaka 2024.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay alisema uamuzi huo wa AU unatoa ishara kubwa kwamba kuwekeza kwenye elimu ni chachu ya kuhimiza maendeleo endelevu barani Afrika, na kuzingatia mahitaji ya vijana.

Kwa mujibu wa UNESCO, kwa sasa watoto milioni 98 waliofikisha umri wa kwenda shule barani Afrika bado hawajapata elimu, na asilimia 90 ya wale walioko shule hawajui kusoma wala kuandika hadi wanapofikia umri wa miaka 10.

Azoulay aliongeza kuwa UNESCO inadhamiria kuunga mkono jitihada za nchi za Afrika katika kutimiza elimu ya msingi na sekondari, na kupata fursa za elimu ya juu yenye ubora na utafiti huko Afrika.