Karibu wakimbizi 100 wa Burundi waliokuwa Rwanda warejea nyumbani
2024-02-22 09:17:44| CRI

Takriban wakimbizi 96 wa Burundi, ambao wengi wao walikimbilia Rwanda mwaka 2015 kutokana na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa, wamerejeshwa makwao.

Kiongozi wa kambi ya wakimbizi ya Mahama Andres Vuganeza amesema kuwa kundi hilo linajumuisha watu 78 kutoka Kambi hiyo, na wengine kutoka Kigali, mji mkuu wa Rwanda. Walikabidhiwa kwa mamlaka za Burundi kwenye mpaka wa Rwanda na Burundi huko Nemba. Ameongeza kuwa wale waliorejeshwa waliamua kurejea Burundi kwa hiari yao.

Burundi ilifunga mpaka wake na Rwanda mwezi Januari, ikisema ni jibu kwa madai ya kwamba Rwanda imeliunga mkono kundi lake la waasi la Red Tabara, linalolaumiwa kwa shambulizi la mwezi Disemba ambapo watu 20 waliuawa kwenye mpaka wa magharibi wa Burundi na DRC. Hata hivyo Vuganeza amesema kufungwa kwa mpaka hakuathiri urejeshwaji.

Urejeshaji wa wakimbizi hao uliwezeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).