Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Jamhuri ya Kongo Denis Sassou Nguesso wamepeana pongezi jana Alhamisi za kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, na kuahidi kuungana na Sassou katika kukuza ushirikiano wa kimkakati wa pande hizo mbili.
Xi alisema katika kipindi cha miaka 60, licha ya mabadiliko ya hali ya kimataifa, nchi hizo zimekuwa na ushirikiano wa dhati na maendeleo ya pande zote mbili, ambapo zimekuwa marafiki wazuri wanaoaminiana kisiasa na wenza wazuri kwa ushirikiano wa kunufaishana wa kiuchumi.
Amebainisha kuwa katika miaka ya hivi karibuni, mawasiliano ya mara kwa mara kati ya nchi hizo mbili, kuendelea kuaminiana kisiasa, na maendeleo thabiti ya ushirikiano wa kivitendo yameleta manufaa yanayoonekana kwa watu wa nchi hizo mbili, jambo ambalo linaonesha waziwazi moyo wa ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika.
Naye rais Sassou alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia, watu wa nchi zote mbili daima wameungana na kuwa rafiki, wakidumisha matarajio ya pamoja ya amani, haki na ustawi. Mambo haya yamehimiza maendeleo ya haraka ya ushirikiano wa kina wa kimkakati kati ya Jamhuri ya Kongo na China.