Gharama ya juu ya kuhamisha fedha ndani ya Afrika Mashariki yazorotesha Soko la Pamoja
2024-02-26 14:05:59| cri

Wananchi wa Afrika Mashariki bado wanasumbuka kupata njia nafuu za kutuma pesa kutoka nchi moja hadi nyingine ndani ya kanda hiyo, hali ambayo imekuwa moja ya vikwazo vikubwa vya biashara huku ikizorotesha utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja.

Takwimu za hivi karibuni kutoka Benki ya Dunia zinaonesha kuwa licha ya jitihada za kupunguza gharama za miamala ili kurahisisha biashara, baadhi ya njia za kutuma pesa katika kanda hiyo ni miongoni mwa njia za gharama kubwa zaidi duniani, na ni za juu zaidi kuliko wastani wa kimataifa.

Wasomi na viongozi wa biashara wanasema hiki kinakuwa moja ya vikwazo vikubwa vya kutimiza kikamilifu muhimili wa soko la pamoja la mafungamano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na hivyo kuchelewesha mihimili mingine ya jumuiya hiyo.