Mwanariadha Mkenya Charles Kipsang afariki muda mfupi baada ya kuvuka mstari wa mwisho katika mbio za Milimani za Cameroon
2024-02-26 23:05:29| cri

Kwa mara nyingine tena maafa yameikumba jamii ya wanariadha baada ya mwanariadha wa Kenya Charles Kipsang kufariki katika mbio za Matumaini za Milimani za Cameroon. Kipsang alianguka na kufariki muda mfupi baada ya kuvuka mstari wa kumalizia katika mashindano ya 29 ya mbio zilizofanyika katika uwanja wa Molyko. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa akiongoza mapema katika mbio lakini alimaliza katika nafasi ya 16 katika kitengo cha Wanaume Wakubwa.

Wahudumu wa afya walimkimbilia kumsaidia, lakini licha ya jitihada zao kubwa, hawakuweza kumfufua. Taarifa zinaonesha kuwa mamlaka tayari ilikuwa imekabidhi zawadi kwa washindi wakati mwanariadha huyo alipothibitishwa kufariki katika Hospitali ya Mkoa ya Buea. Tukio hilo liliwaacha watazamaji na washindani wenzake wakiwa na mshangao na huzuni.