Usambazaji wa umeme wa Afrika Mashariki unatarajiwa kuongezeka mara tu Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) utakapoanza kufanya kazi.
Katika Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Nishati uliofanyika jijini Arusha, Mawaziri hao walisema mradi wa kuzalisha Megawati 2,115, wenye thamani ya Dola bilioni 2.9 katika Mto Rufiji utaleta mabadiliko makubwa katika kanda hiyo. Mradi huo ni sehemu ya mpango mkuu wa umeme wa Tanzania, unaolenga kuunganisha gridi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia.
Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Shaib Hassan Kaduara alisema nishati ina mchango mkubwa katika kuendeleza viwanda na kukuza uwekezaji, hivyo mradi huu ni hatua muhimu ambayo itapunguza nakisi ya umeme sio tu nchini Tanzania bali katika kanda mzima.
Benki ya Dunia inasema kuwa mtu mmoja kati ya wawili katika Afrika Kusini mwa Sahara alikosa umeme mwaka 2023.