Kundi la M23 laanzisha upya mapigano karibu na mji muhimu mashariki mwa DRC
2024-02-27 08:43:06| CRI

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema kundi la waasi la M23 limeanza tena mapigano kwenye viunga vya mji wa Sake, jimbo la Kivu Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Bw. Dujarric amesema ujumbe wa kulinda amani unaripoti kwamba baada ya utulivu wa muda mfupi, jumapili kulitokea mapigano mapya na makali kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa Kongo, magharibi mwa mji wa Sake.

Wakati wa mapigano hayo makombora mawili yalitua karibu na kambi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Kimoka, takriban kilomita 4 kaskazini magharibi mwa Sake. Hakuna majeruhi katika upande wa Umoja wa Mataifa walioripotiwa.

Bw. Dujarric amesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kama MONUSCO, unaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na uhasama unaoendelea mashariki mwa DRC na umesisitiza wito wake kwa kundi la M23 kuacha mashambulizi yake na kuheshimu makubaliano ya Luanda.