Mjumbe maalum wa rais Xi Jinping wa China ahudhuria mazishi ya kitaifa ya rais wa zamani wa Namibia Hage Geingob
2024-02-27 08:38:11| cri

Kuanzia tarehe 24 mwezi huu hadi tarehe 25, mjumbe maalum wa rais Xi Jinping wa China Bw. Jiang Zuojun alihudhuria mazishi ya marehemu rais Hage Geingob huko Windhoek, Namibia, na kutoa hotuba katika hafla ya kumbukumbu. Mchana wa tarehe 25, rais mpya wa Namibia Nangolo Mbumba, alikutana na Jiang Zuojun katika Ikulu ya Namibia.

Jiang Zuojun amewasilisha salamu za rambirambi za Rais Xi Jinping kwa Rais Mbumba, na kwa serikali na watu wa Namibia. Bw. Jiang amesema, China na Namibia zina urafiki mkubwa wa jadi, na katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali umedumisha kasi ya maendeleo. China inatilia maanani sana uhusiano kati ya China na Namibia na inapenda kufanya kazi na Namibia ili kuzidisha uaminifu wa kisiasa na ushirikiano wa kirafiki na kuhimiza kuzidisha na kuimarika kwa ushirikiano wa kimkakati wa kina kati ya nchi hizo mbili.

Bw. Mbumba amemshukuru kwa dhati rais Xi Jinping kwa kutuma mjumbe maalum wa kutoa salamu za rambirambi, na kusisitiza kuwa Namibia inapenda kushirikiana na China kuenzi urafiki wa Namibia na China, kuimarisha ushirikiano katika biashara, uwekezaji, kilimo, sayansi na teknolojia na nyanja nyinginezo, na kuboresha zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ili kunufaisha nchi hizo mbili na watu wake.