Rais Tshisekedi asema yuko tayari kukutana na Rais Kagame kujadili mgogoro wa mashariki mwa DRC
2024-02-28 08:53:08| CRI

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ameeleza nia yake ya kukutana na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, ili kukabiliana na machafuko yanayoendelea mashariki mwa DRC.

Kauli hii imekuja wakati wa ziara ya Rais Tshisekedi mjini Luanda ambako alikutana na Rais wa Angola Joao Lourenco. Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Bw. Tete Antonio amedokeza hilo kufuatia mkutano kati ya marais Lourenco na Tshisekedi.

Bw. Antonio amesema kuwa Rais Lourenco ambaye ni kaimu mpatanishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika, alifanya mazungumzo na Marais Tshisekedi na Kagame wakati wa Mkutano wa 37 wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia. Angola imepewa jukumu la kuwezesha mkutano kati ya viongozi hao wawili, ingawa tarehe maalum bado haijatajwa.

Juhudi za upatanishi zinakuja kufuatia ongezeko la hivi karibuni la migogoro mashariki mwa DRC, unaolihusisha kundi la M23, na nia ya kurejesha uhusiano mzuri kati ya DRC na Rwanda.