Msomi wa Nigeria: China ni mwenzi asiye na mbadala kwa maendeleo ya Afrika
2024-02-29 14:59:12| CRI

Mkutano wa tisa wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utafanyika mwaka huu nchini China, na unatarajiwa kuweka mipango mipya ya ushirikiano wa pande hizo mbili katika siku zijazo. Akizungumzia mfumo huo wa ushirikiano, mtafiti wa Taasisi ya Amani na Utatuzi wa Migogoro ya Nigeria Dkt. Olalekan Babatunde amesema, China ni mwenzi asiye na mbadala kwa maendeleo ya Afrika.

Dkt. Babatunde amesema, mifumo mbalimbali ya ushirikiano iliyoanzishwa na China kama vile FOCAC na “Ukanda Mmoja, Njia Moja”(BRI) imeleta nafasi nyingi za ajira kwa Afrika, kuisaidia Afrika kuhakikisha usalama wa chakula na nishati, na kuhimiza ukuaji wa uchumi wake. Amesema nchini Nigeria na katika nchi nyingine za Afrika, bidhaa zenye ubora wa juu na bei nafuu zilizotengenezwa China zinaonekana kila mahali, na maisha ya watu wa Afrika yameboreka kihalisi kutokana na ushirikiano na China.

Dkt. Babatunde amesema, misaada au mikopo mingi iliyoahidiwa na baadhi ya nchi za magharibi kwa Afrika ama ni ahadi hewa, ama inaambatana na masharti magumu. Zaidi ya hayo, bidhaa za nchi za magharibi zina bei ghali, ambazo watu wa kawaida wanashindwa kumudu. Amesema, bila ushirikiano na China, ongezeko la uchumi wa nchi za Afrika litakabiliwa na gharama kubwa zaidi, hali itakayoleta athari kubwa hasi kwa sekta mbalimbali za nchi hizo ikiwemo viwanda na kilimo.

Msomi huyo amesisitiza kuwa Afrika na China ni ndugu wazuri na wenzi wazuri wakati wa dhiki na faraja, na wana urafiki mkubwa na maelewano ya kina. Afrika na China zinapaswa kuendeleza ushirikiano wa pande mbili na wa pande nyingi kwa moyo wazi zaidi, ili kuinua zaidi ubora na kiwango cha ushirikiano kati yao.