Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy kutembelea Dar
2024-02-29 11:11:54| cri

Waziri mkuu wa Ethiopia, Dk Abiy Ahmed Ali, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu kuanzia leo Februari 29. Ziara yake inatokana na mwaliko maalum wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia ziara hiyo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alisema Dk Abiy atapokelewa rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam Machi 1, 2024 na mwenyeji wake, Rais Samia. Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Waziri huyo alisema ushirikiano baina ya nchi hizo mbili unahusu masuala ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni, usafiri wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa wahamiaji haramu, ulinzi na usalama.

Waziri Mkuu Abiy na ujumbe wake wataondoka Tanzania kurejea Ethiopia Machi 2, 2024.