Sudan Kusini yasema utekelezaji wa makubaliano ya amani unaendelea vizuri licha ya changamoto
2024-02-29 09:00:20| CRI

Sudan Kusini imesema imepata maendeleo ya kutia moyo katika utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yaliyohuishwa, licha ya changamoto kubwa kabla ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2024.

Waziri wa Habari, Mawasiliano, Teknolojia na Huduma za Posta Bw. Michael Makuei Lueth, amesema pamoja na kwamba utekelezaji wa makubaliano ya amani unaweza kuwa wa polepole, serikali imedumisha amani na usalama nchini kote isipokuwa katika maeneo machache yenye migogoro ya kijamii, wizi wa ng'ombe na uporaji.

Amesema licha ya changamoto zinazohusiana moja kwa moja na migogoro ya ndani na udhaifu wa taasisi, serikali ya Sudan Kusini inaendelea kupiga hatua thabiti katika utekelezaji wa makubaliano yaliyohuishwa kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Sudan Kusini.