Tanzania yaunga mkono mifumo ya biashara ya pande nyingi
2024-03-01 10:37:55| cri

Tanzania imesema inaunga mkono mfumo wa biashara ya pande nyingi unaozingatia kanuni ambao unatoa ulinzi na fursa kwa nchi wanachama wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), hasa zile zilizo na maendeleo duni, ndogo na zilizo katika mazingira magumu katika wakati huu muhimu ambapo uchumi wa dunia unaendelea kukabiliwa na hali ya sintofahamu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Tanzania Dk Hashil Abdallah, katika Mkutano wa 13 wa Mawaziri unaoendelea Abu Dhabi, Falme za Kiarabu. Ameongeza kuwa wanaamini WTO ina jukumu kubwa la kuhakikisha maendeleo endelevu ya kimataifa yanapatikana. Aidha amesema katika wakati huu,wana fursa ya kukuza mfumo wa biashara wa kimataifa wenye mwelekeo sahihi kwa kuongeza ufanisi wa WTO kutekeleza majukumu yake, ikianzia na kutathmini utekelezaji wa maamuzi ya awali ya mawaziri.

Alisema mageuzi ya WTO Tanzania yanahakikisha uwiano wa maslahi ya wanachama kwa kuzingatia zaidi kusaidia nchi zinazoendelea na nchi zenye maendeleo duni ili kufikia lengo pana la ushirikishwaji na kuhimiza maendeleo endelevu kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Marrakesh wa kuanzisha shirika la biashara.