Shirika la ndege la Ethiopia limezindua kituo kipya cha ugavi wa biashara ya mtandaoni mjini Addis Ababa, ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wanunuzi na wauzaji reja reja mtandaoni.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi iliyofanyika jana waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Ethiopia Alemu Sime, amesema kituo hicho kinalenga kurahisisha utendaji na usimamizi kabla ya bidhaa kutumwa kwa wateja. Kituo hicho kilichojengwa na kampuni ya China, kina eneo la takriban mita za mraba 15,000 na kina uwezo wa kushughulikia tani laki 1.5 za bidhaa kwa mwaka.
Ofisa Mkuu mtendaji wa Shirika la Ndege la Ethiopia Bw. Mesfin Tasew amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho baada ya ujenzi wa miaka miwili, kunathibitisha kujitolea kwa shirika hilo la ndege kuendana na ubunifu na teknolojia zinazoibukia, na kuimarisha utoaji wa huduma zake.