Uganda yashinda zabuni ya kuandaa Mkutano wa wanasayansi 500 wa kilimo cha bustani mwaka 2028
2024-03-01 10:38:28| cri

Uganda imeshinda zabuni ya kuandaa Mkutano wa 6 wa kilimo cha bustani wa Afrika (AAHC) ambao utafanyika mwaka 2028 huku zaidi ya wajumbe 500 kutoka kote duniani wakitarajiwa kukusanyika Kampala kujadili uboreshaji wa kilimo cha bustani.

Tangazo hilo lilitolewa juzi Jumatano na Mwenyekiti wa Jamii ya Kimataifa ya Sayansi ya Kilimo cha Bustani (ISHS) Profesa Francois Laurens katika mkutano wa kilimo cha bustani (AAHC) unaofanyika huko Marrakech Morocco, na kutarajiwa kumalizika leo Machi Mosi.

Awali mkutano huo uliwahi kufanyika katika nchi za Kenya, Afrika Kusini, Nigeria, Senegal na sasa mwaka huu wa 2024 unafanyika nchini Morocco.

Wajumbe watakaohudhuria mkutano ujao wa Uganda wa mwaka 2028 ni pamoja na wanasayansi, watafiti, wawekezaji wa makampuni na sekta binafsi kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo kutoka Afrika na maeneo mengine duniani.