Mara nyingi binadamu, hususan wanawake, wamekuwa makini sana na miili yao, wengine wakiamini kwamba wembamba ndio uzuri na wengine wakijali zaidi afya kuliko umbile. Lakini kama ilivyo kawaida kwa binadamu, kuridhika ni jambo ambalo kwa kiasi fulani haliwezekani, maana kama ni mnene utataka kuwa mwembamba, na kama mwembamba utataka kuwa mnene, kama mweusi utataka kuwa mweupe, na kama mweupe utataka kuwa mweusi. Hii ni kawaida ama tuseme ni desturi ya mwanadamu.
Hiyo ni kweli. Lakini katika siku za karibuni kumeibuka tabia ya watu ambao wamezidi unene kutumia dawa za kupunguza mwili, ambazo wakati mwingine zinakuwa na athari mbaya kwa mwili wa mwanadamu. Wengine wanapunguza mwili kwa kuacha kula vyakula fulani na kuongeza ulaji wa vyakula fulani, ilimradi tu apate matokeo anayotaka. Lakini jambo ambalo wengi tunalisahau katika jitihada za kupunguza uzito, ni kwamba kila chakula kina faida yake mwilini, isipokuwa tu, kitumike kwa kiasi. Sasa leo katika kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake, tutaangazia njia za asili za kupunguza uzito.