Wanachama wa OPEC+ kupunguza zaidi uzalishaji wa mafuta katika robo ya pili ya mwaka
2024-03-04 08:39:57| CRI

Nchi kadhaa wanachama zinazozalisha mafuta duniani na washirika wao OPEC+ zimetangaza kupunguza zaidi uzalishaji wa mafuta katika robo ya pili ya mwaka ili kusaidia "utulivu na usawa wa masoko ya mafuta."

OPEC ilisema Jumapili usiku kwamba Sekretarieti yake "ilibaini matangazo" ya nchi kadhaa za OPEC+ kupunguza kwa hiari uzalishaji wa jumla ya mapipa milioni 2.2 kwa siku (bpd) katika robo ya pili ya 2024.

OPEC imesema hatua hii ya kupunguza uzalishaji imechukuliwa kutoka kwenye mgawo uliopitishwa katika mkutano wa mawaziri wa OPEC+ Juni mwaka 2023. Ni nyongeza ya kupunguza uzalishaji kwa hiari uliotangazwa na nchi za OPEC+ Aprili mwaka jana na baadaye kuongezwa muda hadi mwishoni mwa 2024.

Hata hivyo, taarifa ya OPEC ilibainisha kuwa upunguzaji huu wa hiari "utaondolewa hatua kwa hatua kulingana na hali ya soko" ili kusaidia utulivu wa soko baada ya mwezi Juni.