Kenya yapokea mabehewa mapya kutoka China kwa ajili ya shughuli za kusafirisha mizigo kwa njia ya reli
2024-03-05 08:48:09| CRI

Kenya ilipokea mabehewa 430 kutoka China Jumatatu ili kuimarisha shughuli za usafirishaji wa mizigo kwenye mtandao wake wa reli nchini kote. Shehena hiyo inajumuisha mabehewa 230 yaliyotengenezwa kwa ajili ya reli ya kasi ya SGR iliyojengwa na China na mabehewa 200 kwa ajili ya reli ya kawaida ya MGR.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Barabara na Uchukuzi, Mohamed Daghar, alisema mabehewa hayo yatarahisisha uondoaji wa mizigo kutoka bandari ya Mombasa na kusaidia kupunguza msongamano barabarani. Ameongeza kuwa mabehewa yote yana uwezo wa kubeba tani 70 au zaidi, hivyo kuwezesha usafirishaji wa mizigo mizito ambayo inapunguza uharibifu wa barabara.

Kuwasili kwa mabehewa hayo mapya kunakuja chini ya mwezi mmoja baada ya Kenya kupokea mabehewa mapya 50 kutoka China mwezi Februari ili kurahisisha shughuli za huduma ya mizigo za reli ya SGR.