China yaanza vikao viwili vya mwaka kwa dhamira ya kuimarisha ukuaji wa uchumi
2024-03-05 08:54:58| CRI

Vikao viwili vya mwaka vya China vimeanza rasmi jana Jumatatu kufuatia kufunguliwa kwa kikao cha pili cha Kamati Kuu ya 14 ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China, CPPCC.

China ikiwa ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani, huku ikijitahidi kuimarisha ukuaji wa uchumi na kuwa mbioni kuelekea kuwa nchi ya kisasa, vikao hivyo viwili vinabeba umuhimu mkubwa kwa China na zaidi.

Kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati kuu ya CPPCC kinachowaleta pamoja washauri wa kisiasa zaidi ya elfu mbili kutoka sekta mbalimbali za jamii, mwenyekiti wa kamati hiyo Wang Huning ametoa ripoti ya kazi akisema mwaka huu CPPCC itazingatia kusukuma mbele juhudi za China za kujijenga kuwa nchi ya kisasa, kutoa ushauri na kuhimiza maafikiano mapana, ili China iweze kutimiza malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mwaka huu.