EU yatenga fedha kusaidia Tanzania kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu
2024-03-05 08:47:31| CRI

Umoja wa Ulaya (EU) umetoa taarifa ukisema umetenga euro 150,000 (kama dola za Kimarekani 162,919) za msaada wa kibinadamu kwa Tanzania ili kukabiliana na janga la hivi karibuni la kipindupindu nchini humo.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa msaada huo unalenga kusaidia Tanzania kudhibiti mlipuko huo, ambao unahatarisha zaidi ya watu milioni 4. Pia ilisisitiza kuwa ufadhili wa EU utaimarisha juhudi za Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania katika kutoa misaada inayohitajika zaidi, ikiwemo maji safi, huduma za afya na usafi. Ufadhili huo utakaoendelea kwa muda wa miezi mitatu hadi mwisho wa Mei 2024, unatarajiwa kuwafikia watu 178,000 katika maeneo yaliyoathirika zaidi katika mikoa ya Kagera, Mwanza na Shinyanga.

Kwa sasa Tanzania inakabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu katika takriban miaka 40, huku mikoa 13 ikiathirika tangu mapema Januari 2024. Janga hili lililoenea linazidishwa na mvua kubwa ya El Nino, ambayo inaelemea mifumo ya maji taka na miundombinu mingine, haswa katika maeneo yenye watu wengi.