Usalama wa kijamii na majumbani wa wanawake
2024-03-08 08:00:14| CRI

Hivi sasa Mikutano Miwili ya China inaendelea, ambapo wawakilishi na wajumbe kutoka mikoa na sekta mbalimbali wamekusanyika mjini Beijing, kutoa mapendekezo kuhusu maendeleo ya nchi na kuboresha maisha ya watu.

Katika mikutano hiyo, mambo ya wanawake ni mada muhimu, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa haki na usalama wa wanawake majumbani. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirikisho la Wanawake la China mwaka 2002, asilimia 30 ya familia milioni 270 za China zinakabiliwa na unyanyasaji majumbani, ambapo waathirika hao wanahitaji sheria na sera za kulinda haki zao za kisheria na usalama binafsi. Kutokana na utafiti wa miaka mingi na juhudi za wajumbe wa Mikutano Miwili, tarehe 27 Desemba mwaka 2015, Kamati ya Kudumu ya Bunge la Umma la China imepitisha Sheria ya Kupambana na Unyanyasaji na Ukatili wa Majumbani, ikiashiria hatua mpya katika juhudi za China za kupinga unyanyasaji wa majumbani kwa mujibu wa sheria. Na sheria hiyo imekuwa ikizidi kuboreshwa. 

Tukiangazia barani Afrika, suala la mauaji ya wanawake nchini Kenya, sasa limekuwa mada nzito ambayo hadi sasa bado haijapatiwa ufumbuzi. Wanawake wengi wamejikuta wakiwa wanatembea huku wakiangalia begani kwao kwa hofu ya kuvamiwa, kuchukuliwa mateka, kwenda kubakwa na hatimaye kuuliwa. Tatizo hili limeyafanya mashirika ya kutetea haki za binadamu sasa kuitaka Serikali ya Kenya, kuchukua hatua za makusudi kuanzisha uchunguzi na kuwashtaki watu wanaotuhumiwa kwa makosa ya mauaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake. Hivyo kwa kuzingatia ukali wa tatizo hili Ukumbi wa Wanawake leo utaangazia Usalama wa kijamii na majumbani wa wanawake.