Rwanda imewasilisha ombi kwa Umoja wa Afrika ikiutaka usiunge mkono majeshi yaliyotumwa na nchi za kusini mwa Afrika huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na kudai kuwa majeshi hayo yatazidisha migogoro nchini humo.
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta amesema kwenye barua kwa mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat kwamba Rwanda ina wasiwasi mkubwa na mkutano utakaofanywa na Baraza la Amani na Usalama la AU, ambao moja ya malengo yake ni kuidhinisha kupelekwa kwa jeshi la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika nchini DRC (SAMIDRC) na kutathmini msaada unaoweza kutolewa kwao.
Bw. Biruta ametaka Umoja wa Afrika usiunge mkono wala kufadhili SAMIDRC akishutumu jeshi hilo kufanya mapambano pamoja na jeshi la DRC na makundi mengine ya muungano ya wanamgambo likiwemo kundi la waasi wa Rwanda FDLR, na kudai jumuiya hiyo inazingatia suluhisho la kijeshi linalokwenda kinyume na moyo wa mapendekezo yote ya amani ya kikanda.