Rais Samia atenga siku moja kila mwezi kusikiliza kero za wananchi
2024-03-06 13:42:07| cri

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda, ametangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametenga siku moja kila mwezi kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi yeye mwenyewe katika ofisi za chama hicho zilizopo Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.

Akiwa Mkuu wa nchi na mwenyekiti wa chama tawala, Rais Samia analenga kushirikiana moja kwa moja na wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

Bw Makonda amesema mikutano hiyo itawapa wananchi fursa ya kueleza changamoto zao moja kwa moja kwa Rais.

Bw. Makonda amesema uamuzi huo wa Rais Hassan unachangiwa na mazoea ya aliyekuwa Rais, Marehemu Ali Hassan Mwinyi, ambaye katika kipindi chake cha urais na uenyekiti wa CCM, mara kwa mara alitenga siku moja kila mwezi kukutana na wananchi katika ofisi za CCM-Lumumba kusikiliza kero za wananchi.