Mkutano wa Nishati wa Afrika waangazia matarajio ya ushirikiano wa nishati kati ya Afrika Kusini na China
2024-03-07 08:37:42| CRI

Mkutano wa Nishati wa Afrika wa 2024 unaoendelea mjini Cape Town, nchini Afrika Kusini, umetoa mwanga kuhusu matarajio ya ushirikiano wa nishati kati ya Afrika Kusini na China, huku Waziri wa Rasilimali ya Madini na Nishati wa Afrika Kusini Gwede Mantashe akisisitiza uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili.

Ukiwa chini ya kaulimbiu "Mabadiliko ya Nishati ya Afrika kutoka Matarajio hadi Hatua- Kutoa Mustakabali Endelevu na wenye Mafanikio," mkutano huu wa 16 unalenga kuchunguza njia za kukuza maendeleo ya nishati mbadala barani Afrika.

Akiulizwa kuhusu ushirikiano wa nishati kati ya Afrika Kusini na China katika mkutano na wanahabari Jumanne, Mantashe alisema China ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Afrika Kusini na nchi hizo mbili zina uhusiano mzuri. Akibainisha kuwa China na Afrika Kusini ni wanachama wa kundi la BRICS, alisisitiza umuhimu wa kudumisha na kuimarisha uhusiano na China na nchi nyingine ndani ya mfumo huo.

Mkutano huo wa siku tatu unawaleta pamoja maafisa wa serikali, wataalam wa sekta, waendelezaji wa mradi, watumiaji wa nishati, na watengenezaji ili kujadili na kutafuta suluhu ya kudumu ya mabadiliko ya nishati.