Viongozi wa China na Afrika watakutana tena Beijing kujadili mipango ya maendeleo na ushirikiano wa siku zijazo
2024-03-07 11:38:39| cri

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi amesema hivi sasa, “dunia ya kusini” inayowakilishwa na China na Afrika inashamiri na ina athari kubwa katika historia ya dunia. Katika mchakato huu mpya wa kihistoria, China itaendelea kusimama kidete na ndugu wa Afrika, kuunga mkono Afrika katika kupata uhuru halisi kimawazo, kuisaidia Afrika kuboresha uwezo wake wa kujiendeleza kwa kujitegemea, na kuiunga mkono Afrika katika kuharakisha mchakato wake wa kisasa.

Amesema China daima imekuwa ikisisitiza kuwa Afrika haipaswi kutengwa. Baada ya ushirikiano kati ya China na Afrika kushamiri, nchi nyingine kubwa pia zimeelekeza tena nguvu zao kwa Afrika, na China inakaribisha hali hiyo. China inatumai kuwa pande zote, kama China, zitazingatia zaidi Afrika, kuongeza uwekezaji barani Afrika, na kusaidia maendeleo ya Afrika. Pia China iko tayari kufanya ushirikiano zaidi wa pande tatu na wa pande nyingi kwa msingi wa kuheshimu matakwa ya Afrika.

Bw. Wang Yi amesema mkutano mwingine wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utafanyika nchini China mwaka huu, ambapo viongozi wa China na Afrika watakutana tena Beijing baada ya miaka sita kujadili mipango ya ushirikiano wa maendeleo ya siku zijazo na kubadilishana uzoefu wa kina katika utawala wa nchi.