WHO yafanya mkutano wa mawaziri nchini Cameroon unaohusu kuzuia malaria
2024-03-07 08:39:59| CRI

Shirika la Afya Duniani (WHO) na washirika wake Jumatano waliitisha mkutano wa mawaziri mjini Yaounde nchini Cameroon ambao unahusu namna ya kukabiliana na ugonjwa wa malaria katika nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo.

Akiongoza hafla za ufunguzi, Waziri Mkuu wa Cameroon Joseph Dion Ngute alisema ni muhimu kuunganisha rasilimali ili kuzuia watu kufa kutokana na ugonjwa wa malaria ambao bado ni muuaji namba moja katika nchi nyingi za Afrika.

Kwa mujibu wa WHO uhaba wa fedha unasalia kuwa kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya malaria, huku pengo la ufadhili kati ya kiasi kilichowekezwa na rasilimali zinazohitajika, limefikia dola za kimarekani bilioni 3.7 mwaka 2022. 

WHO ilisema katika taarifa yake kwamba mkutano huu wa Mawaziri unalenga kuimarisha ahadi za kisiasa na kifedha kwa ajili ya kukabiliana na malaria kwa kasi, kwa nia ya kufikia malengo ya GTS 2030. Utaweka mwongozo wa kuongeza dhamira ya kisiasa na ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti malaria, kwa utaratibu wazi wa uwajibikaji.