Katibu mkuu wa UM atoa mwito wa kusitisha uhasama nchini Sudan wakati wa Ramadhani
2024-03-08 08:58:21| CRI

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres ametoa mwito wa kusitisha uhasama katika mwezi mtukufu wa Ramadhani nchini Sudan.

Bw. Guterres amehimiza pande zote nchini Sudan kuheshimu thamani ya Ramadhani kupitia kusitisha uhasama wakati wa Ramadhani. Kusitishwa kwa uhasama kunapaswa kupelekea kunyamazisha bunduki kabisa kote nchini na kutandika njia imara inayoelekea amani ya kudumu kwa watu wa Sudan.

Wakati huohuo, Baraza la Mpito la Mamlaka ya Sudan limetoa taarifa ikisema, nchi hiyo itafanya juhudi kuendelea na uratibu wa Umoja wa Mataifa, ili kuhakikisha msaada wa kibinadamu unawafikia watu wanaoathiriwa na vita vinavyoendelea.

Taarifa hiyo imetolewa baada ya Kamati ya Kitaifa ya Sudan ya Kukabiliana na Dharura za Kibinadamu kukutana huko Port Sudan, mji mkuu wa jimbo la Bahari ya Sham, huku ikibainisha kuwa mkutano huo umejadili kuhusu kufungua kivuko cha mpaka wa magharibi na Chad, kivuko cha mpaka na Sudan Kusini kupitia mji wa Kosti na vivuko vya mpaka vya Ashkit na Arqin kaskazini mwa Sudan.