Sekta ya fedha ya Tanzania inaendelea kuwa imara
2024-03-08 08:33:13| CRI

Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango amesema sekta ya fedha ya nchi hiyo inaendelea kuwa imara dhidi ya athari mbalimbali zilizopo duniani.

Akiongea kwenye Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania ikishirikiana na benki nyingine, Mpango amesema sekta ya fedha ya Tanzania imekuwa na utendaji mzuri, ikikua kwa asilimia 22 katika mwaka 2022/2023 ikilinganishwa na ukuaji wa karibu asilimia 10 katika mwaka 2021/2022.

Mpango amewataka wajumbe zaidi ya 1,000 waliokutana Arusha kujadili kwa kina maeneo yanayotishia na yanayoleta changamoto kwenye sekta ya fedha kutokana na kukatizwa kwa biashara duniani, ambako kunasababishwa na mnyororo wa usambazaji wa vitu, migogoro ya siasa za kijiografia na mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema bado kuna changamoto nyingi duniani, hivyo wadau hao wanapaswa kuziangalia tena sheria na kanuni ili kuwezesha sekta hiyo kuboreka zaidi.