Kundi lenye silaha lawateka nyara makumi ya watu kaskazini mwa Nigeria
2024-03-08 08:45:13| CRI

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa makumi ya wakimbizi wa ndani katika jimbo la kaskazini la Borno nchini Nigeria wametekwa nyara hivi karibuni na kundi lenye silaha.

Kwenye taarifa iliyotolewa jana mjini Abuja, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na wa misaada ya kibinadamu nchini Nigeria Mohamed Fall amesema inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 200 wanaotafuta hifadhi katika kambi ya wakimbizi wa ndani kwenye eneo la Ngala jimboni Borno walitekwa nyara na kundi lenye silaha wakati walipokuwa wakiokota kuni Februari 29.

Umoja wa Mataifa umelaani vikali utekaji nyara huo wa wakimbizi wa ndani, ambao wengi wao ni wanawake na watoto, na kutoa wito wa kuachiliwa kwao mara moja. Umoja huo pia umezikumbusha pande zote kwenye mgogoro zitekeleze wajibu wao kwa mujibu wa sheria ya kibinadamu ya kimataifa.