Mashirika ya UM yahimiza msaada wa kimataifa kwa Wasomali waliokumbwa na mgogoro
2024-03-08 08:41:47| CRI

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura katika Ofisi ya Uratibu wa Mambo ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) Bi. Joyce Msuya na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Bi. Beth Bechdol wamewasili nchini Somalia Alhamisi wiki hii, ambapo watafanya ziara ya siku tatu kwa ajili ya kuhimiza kuendelea kutolewa msaada wa kimataifa kwa Wasomali wanaoathiriwa na baa la njaa, migogoro na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mashirika hayo, viongozi hao wawili watakutana na watu walioathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya tabianchi, maafisa wa serikali, wafadhili na wafanyakazi wa msaada ili kutafuta njia ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na majanga hayo, pia watasisitiza umuhimu wa kuwapa kipaumbele na kuwawezesha wanawake walioathirika na mgogoro wa kibinadamu nchini humo na kujumuika na wanawake wa Somalia kuadhimisha siku ya wanawake duniani leo Ijumaa.