Idadi ya watalii waliotembelea mbuga za wanyama za Tanzania yaongezeka
2024-03-11 08:41:15| CRI

Msemaji wa Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ya Tanzania Bw. Mobhare Matinyi amesema idadi ya watalii wanaotembelea mbuga 22 za taifa za Tanzania iliendelea kuongezeka katika mwaka uliopita licha ya uharibifu uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha kwa miundombinu ya mbuga nyingi za taifa.

Bw. Matinyi amesema kati ya Julai 2023 na Februari 2024 watalii zaidi ya milioni 1.45 walitembelea Mbuga za Taifa, na mbuga ya Taifa ya Serengeti ikiwa kivutio kikuu.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lilikuwa na lengo la kuwavutia watalii zaidi ya milioni 1.37 kati ya mwaka 2023 hadi 2024. Hata hivyo takwimu za hivi punde zinaonyesha kuwa lengo hili limevukwa.

Mvua kubwa iliyonyesha na kuathiri miundombinu katika hifadhi nyingi za Taifa, haikuzuia watalii, ameongeza na kubainisha kuwa TANAPA inaendelea na kazi ya kukarabati barabara zilizoharibika ili kuhakikisha mtiririko mzuri wa watalii.