Mkutano wa kimataifa wafunguliwa nchini Kenya ili kuhimiza usalama wa chakula
2024-03-12 08:50:31| CRI

Mkutano wa Kimataifa wa siku tano wa kuhimiza usalama wa chakula duniani ulifunguliwa Jumatatu mjini Nairobi nchini Kenya. Mkutano huo wa 54 wa Tume ya Codex kuhusu Usalama wa Chakula umewaleta pamoja zaidi ya washiriki 200 wakiwemo wawakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) pamoja na maafisa wakuu wa serikali kupitia njia za kuondoa hatari za ugonjwa unaotokana na chakula.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo nchini Kenya, Mithika Linturi, alisema usalama wa chakula ni muhimu katika kufikia Malengo kadhaa ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo kutokuwepo kabisa kwa njaa (njaa sifuri), afya na ustawi, maji safi na usafi wa mazingira, na uzalishaji wa kuwajibika.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Codex Alimentarius, ambayo ni chombo cha kiserikali chenye lengo la kutekeleza viwango vya chakula vya FAO na WHO, Steve Wearne, alisema viwango lazima viendelee kuwa msingi wa usalama wa chakula katika ulimwengu unaobadilika ili kuunga mkono juhudi za pamoja za kumaliza njaa na utapiamlo ifikapo 2030.