Zimbabwe yahimizwa kukumbatia ushirikiano wa kimataifa kufuatia kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani
2024-03-12 08:49:14| CRI

Wafanyabiashara wa Zimbabwe wamehimizwa kutafuta fursa za ushirikiano na washirika wa kimataifa baada ya Marekani kuiondolea vikwazo vipana nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Wito huo umetolewa Jumatatu mjini, Harare na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Frederick Shava katika ufunguzi wa mkutano wa Biashara kati ya Zimbabwe na Marekani.

Ujumbe wa watu tisa kutoka Kamati ya Fursa Duniani ya Chama cha wafanyabiashara cha “Atlanta Black Chambers” (ABC), shirika lisilo la faida lenye makao yake mjini Atlanta, Marekani, kwa sasa uko nchini Zimbabwe kuchunguza fursa za uwekezaji nchini humo. Ujumbe huu wa biashara na uwekezaji, ambao ni wa kwanza tangu serikali ya Marekani isitishe mpango wake wa vikwazo kwa Zimbabwe wiki iliyopita, ni sehemu ya ziara ya kikanda inayojumuisha Afrika Kusini na Zambia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wiki iliyopita na Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa ya Zimbabwe, ujumbe wa ABC unatarajiwa kukutana na viongozi kadhaa wakuu wa sekta hiyo wakati wakitafuta fursa za uwekezaji katika mali isiyohamishika, viwanda na usambazaji, bima, TEHAMA, nishati mpya, madini, na sekta za biashara na uwekezaji.