Tanzania yalenga kutekeleza miradi mipya ili kuimarisha ukuaji wa uchumi
2024-03-13 08:40:34| CRI

Mamlaka nchini Tanzania zimesema nchi hiyo inapanga kutekeleza miradi mipya katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 ambayo itaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini na kuongeza mapato ya serikali, hasa fedha za kigeni.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, prof. Kitila Mkumbo amesema utekelezaji wa miradi hiyo mipya umeainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaoanza 2021/2022 hadi 2025/2026.

Mkumbo aliyasema hayo wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwenye mkutano maalum wa wabunge wote unaoendelea mjini Dodoma.

Mkumbo alisema kipaumbele pia kitatolewa katika kuongeza uzalishaji viwandani na kuleta ongezeko la awali la thamani katika sekta za kilimo, uvuvi, misitu na madini.