Kenya yaanza kutoa motisha kwa wawekezaji wa kigeni katika maeneo ya viwanda
2024-03-13 08:41:26| CRI

Katibu mkuu wa Idara ya Taifa ya Viwanda katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda ya Kenya Juma Mukhwana amesema kuwa Kenya imeanza kutoa motisha kwa wawekezaji wa kigeni wanaoanzisha biashara katika maeneo ya viwanda.

Bw. Mukhwana amesema hayo kwenye kongamano la biashara lililofanyika mjini Nairobi nchini Kenya, akiongeza kwamba wawekezaji wa kimataifa watapata faida za kodi, pamoja na kupata ardhi bure na mabanda ya viwanda, ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Mukhwana ameyasema hayo wakati wa maonyesho ya biashara ya Afrika Mashariki ya Propak 2024 na mkutano wa vifungasho, na kuongeza kuwa malighafi zinazotumika katika maeneo ya viwanda pia zitaagizwa bila kutozwa ushuru. Amesema maeneo ya viwanda pia yatatoa umeme wa gharama nafuu kwa wazalishaji. Ujenzi wa maeneo 18 ya kaunti na maeneo ya viwanda unaendelea nchini kote, na vituo hivi vinatarajiwa kuwezesha ongezeko la thamani ya malighafi zinazopatikana nchini humo.