Pande za makubaliano ya amani ya Ethiopia zathibitisha nia ya kutekeleza makubaliano ya amani kufuatia mkutano wa kimkakati wa AU
2024-03-13 08:42:03| CRI

Umoja wa Afrika (AU) umetoa taarifa ukisema pande zinazohusika kwenye makubaliano ya amani ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili kaskazini mwa Ethiopia wamesisitiza nia yao ya kutekeleza makubaliano ya amani.

Haya yanajiri wakati umoja huo wenye wanachama 55 ulipoitisha mkutano wa kwanza wa kimkakati wa kutafakari juu ya utekelezaji wa Mkataba wa Kusimamisha Uhasama (COHA) nchini Ethiopia siku ya Jumatatu.

Kwa mujibu wa AU mkutano huo wa utekelezaji wa mkataba wa amani uliotiwa saini Novemba 2022 kati ya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) uliitishwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat, ambapo pamoja na mambo mengine, ulilenga kupitia maendeleo yaliyofikiwa, kubainisha changamoto kuu na kupendekeza njia za kukabiliana na mapungufu katika utekelezaji wa COHA.

Ili kutambua maendeleo yaliyopatikana na kutambua maeneo ambayo yanahitaji juhudi za ziada za pamoja katika kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo, pande hizo mbili ziliamua zaidi kushauriana mara kwa mara na kukutana ndani ya miezi michache ijayo.