Mikoa miwili bado imeathiriwa na ugonjwa wa kipindupindu nchini Tanzania
2024-03-13 10:42:55| cri

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu, ametoa tahadhari ya wananchi kuepuka kutiririsha maji taka kuelekea msimu wa mvua za masika, na kuzitaka halmashauri kuweka sheria kali za faini ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy amesema kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu imepungua nchini humo, na kwamba ni mikoa miwili tu iliyoripoti kesi mpya, tofauti na awali ambapo mikoa 10 ilikumbwa na ugonjwa huo, na kutaja mikoa hiyo kuwa ni Mwanza na Simiyu.

Pia amesema, Wizara yake inaendelea kuhimiza wananchi kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira ambapo wiki ijayo  watazindua kampeni itakayojikita kwenye masuala ya afya na mazingira kwani wakiweka mazingira safi na salama wataweza kupambana na kipindupindu.