Rais wa Nigeria aahidi kutolipa fedha ili kuachiliwa kwa wanafunzi na wanawake waliotekwa nyara
2024-03-14 10:32:26| cri

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ameweka wazi msimamo wake thabiti dhidi ya kulipa fedha kwa lengo la kukomboa wanafunzi na wanawake waliotekwa nyara hivi karibuni.

Waziri wa Habari na Mazingira ya Kitaifa, Mohamed Idris ametangaza msimamo huo wa rais wakati akiongea na wanahabari mjini Abuja, na kusisitiza haja ya juhudi za pamoja kati ya mamlaka za usalama ili kuwaokoa waathirika.

Waziri huyo ametilia mkazo ahadi ya serikali ya kufanya kila linalowezekana kwa kushirikiana na wenzi wa kimatafa, huku ikikataa kufanya mazungumzo na makundi ya kihalifu.

Watu wenye silaha wamewateka nyara wanafunzi 287 katika shambulio dhidi ya shule kadhaa katika mkoa wa Kaduna, kaskazini magharibi mwa Nigeria. Tukio hilo limekuja baada ya wanawake kadhaa katika mkoa wa Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria kutekwa nyara mwishoni mwa mwezi Februari.