Nigeria yafungua mipaka ya ardhini na anga na Niger kufuatia azimio la ECOWAS
2024-03-14 09:42:43| CRI

Nigeria Jumatano ilifungua mipaka yake ya ardhini na anga na Jamhuri ya Niger na kuondoa vikwazo vilivyowekwa hapo awali dhidi ya nchi hiyo kufuatia mapinduzi ya kumuondoa Rais Mohamed Bazoum mwaka 2023.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu alitoa agizo hilo kwa kuzingatia maamuzi ya Mamlaka ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) yenye wanachama 15 katika mkutano wake wa Februari 24 huko Abuja, nchini Nigeria.  Katika mkutano huo, viongozi wa Afrika Magharibi walikubaliana kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Niger, Burkina Faso, Guinea na Mali.

Nigeria ilikuwa imefunga mipaka yake ya anga na ardhini na Niger Agosti 2023 huku ikilishawishi jeshi la nchi hiyo kumwachilia huru Bazoum aliyezuiliwa pamoja na watu wa familia yake, na pia kurejesha utaratibu wa kikatiba.