Ethiopia yakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu kutokana na athari za hali ya hewa na milipuko ya magonjwa
2024-03-14 09:45:10| CRI

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (UNOCHA) imeonya kuwa Ethiopia inaendelea kukabiliwa na janga kubwa la kibinadamu linalosababishwa na athari za hali ya hewa, milipuko ya magonjwa na ukosefu wa usalama.

UNOCHA hivi karibuni imetoa taarifa yake kuhusu mwitikio wa kibinadamu wa kipaumbele wa Ethiopia na mapungufu makubwa ya ufadhili, ikisema kuwa mzozo huo wa kibinadamu unazidishwa na changamoto za kiuchumi na kifedha.

Kutokana na hali ngumu ya kibinadamu inayoikabili nchi hiyo ya Afrika Mashariki, UNOCHA imesema kuwa serikali ya Ethiopia, Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu wanaendelea kupitia mazingira magumu, yasiyotabirika na tata ya kibinadamu huku kukiwa na rasilimali chache.

UNOCHA imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa fedha haraka ili kuzuia kuzorota kwa hali ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na maeneo mapya yaliyoathiriwa na ukame unaotokana na El Nino.