Rwanda na Tanzania kufungua mpaka mpya
2024-03-14 09:34:50| CRI

Rwanda na Tanzania zimekubali kufungua mpaka mpya ili kuhimiza biashara na usafiri wa watu kati ya nchi mbili.

Makubaliano hayo yalitangazwa Jumanne mjini Kigali, Rwanda baada ya mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Vincent Biruta na mwenzake wa Tanzania January Yusuf Makamba.

Kwenye mkutano wa pamoja na wanahabari, mawaziri hao wawili walisema nchi mbili zimekubali kufungua mpaka wa pili huko Kyerwa wilayani Ngara, Tanzania. Kwa sasa, Rwanda na Tanzania zina mpaka mmoja unaotambuliwa rasmi huko Rusumo, kilomita takriban 142.2 kusini mashariki mwa Kigali.

Makamba alisema Tanzania itaimarisha ushirikiano na Rwanda kwenye sekta za biashara, teknolojia ya habari na nishati. Kwa upande wa Rwanda, Biruta alisema Tanzania ni jirani mwema na mwenzi muhimu wa biashara wa Rwanda. Pia Biruta alisema walijadili masuala ya usalama wa kikanda na mengine wanayofuatilia kwa pamoja.