Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar watangazwa kuwa mojawapo ya viwanja bora zaidi barani Afrika
2024-03-15 08:51:45| CRI

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume mjini Zanzibar umetangazwa kuwa mojawapo ya viwanja vya ndege bora zaidi barani Afrika.

Akiongea na wanahabari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Seif Abdalla Juma alisema tuzo za kila mwaka za Ubora wa Huduma za Viwanja vya Ndege zinazotangazwa na Baraza la Viwanja vya Ndege vya Kimataifa, zitaongeza ujio wa watalii kutoka nje ya nchi katika Visiwa vya Zanzibar.

Amesema tuzo hizo zinatambua ubora wa uwanja wa ndege kulingana na maoni ya abiria yaliyokusanywa kupitia tafiti za kila siku katika maeneo ya kuondoka na kuwasili duniani kote.

Juma alisema mafanikio hayo yametokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ndio uwanja wa ndege pekee Zanzibar. Kampuni ya Uhandisi wa Ujenzi ya Beijing, inayoongoza nchini China, ilijenga kituo cha tatu cha uwanja wa ndege huo.