Wataalamu wakutana nchini Kenya ili kuongeza uhamaji wa wanafunzi katika Afrika Mashariki
2024-03-15 08:52:46| CRI

Wataalamu wa elimu wa Afrika Alhamisi wameanza mkutano wa siku mbili mjini Nairobi, nchini Kenya ili kujadili njia za kuimarisha uhamaji wa wanafunzi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kongamano la Uhamaji wa Wanafunzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lilileta pamoja zaidi ya makamu wakuu wa vyuo 100 pamoja na wawakilishi kutoka wizara zinazohusika na elimu ya juu ndani ya EAC ili kupitia upya njia za kukuza ubadilishanaji wa wanafunzi na wafanyakazi wa elimu ya juu katika jumuiya hiyo.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, katibu mtendaji wa Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), Gaspard Banyankimbona, alisema kuwa utekelezaji wa eneo la elimu ya juu la EAC utarahisisha uhamisho wa wanafunzi kutoka taasisi moja ya elimu hadi nyingine ya kanda hiyo.

Banyankimbona aliongeza kuwa kwa sasa EAC inaandaa mfumo wa kisheria wa kuhakikisha mifumo ya elimu inaruhusu utambuzi wa vyeti vya taaluma katika kanda nzima na kubainisha kuwa uhamaji wa wanafunzi ni njia mojawapo ya kuongeza ushirikiano wa kikanda kwa kuruhusu uhamishaji wa ujuzi na kazi ndani ya kanda.